Ubalozi wa Tanzania Visiwani Comoro ulitoa mwaliko kwa jopo la wanfanya biashara mashuhuri nchini Tanzania kuja kufanya ziara ya kikazi Visiwani Comoro na kuangalia fursa mbalimbali za masoko kwa ajili ya kuuza bidhaa za Tanzania Visiwani hapa. Ujumbe huo wa wafanyabiashara ulijumuisha watu wafuatao; Bw. Severini Mushi, Bw. Revocatus Niwesi, Bw. Nicholas Mwasumbi na Bw. Emanuel Bagma.
Wakati wakiwa ziarani Visiwani hapa wajumbe walipata fursa ya kufanya vikao na Uongozi wa Chamber of Commerce ya Ngazidja na Anjouan, mkutano huu ulifanyika katika ukumbi wa mkutano wa Ubalozi tarehe 21 Februari, 2019. Chamber of Commerce ya Anjouan walionyesha nia yao ya kutaka kununua bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania ikiwemo vinywaji, nyama, vifaa ya ujenzi n.k. Wajumbe waliweza kuptia (draft MoU) ambayo inatarajiwa kutiwa saini wakati wowote.
Sambamba na hilo, wajumbe walipata fursa pia ya kukutana na Waziri wa Biashara wa Comoro Mhe. Bianrifi Tharmidhi pamoja na Mkurugenzi wake wa Biasahara za nje (External Trade). Mkutano huo ulifanyika katika ofisi za Wizara hiyo na kuhudhuriwa pia na Mhe. Sylvester M. Mabumba, Balozi wa Tanzania Visiwani Comoro.
Katika mkutano huo Mhe. Balozi alichukua fursa hiyo kuhamasisha Serikali ya Comoro kuchangamkia fursa za kufanya biashara baina ya nchi hizi mbili pamoja na Serikali hizo kufanya kazi kwa pamoja kutafuta namna ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara baina ya Tanzania na Comoro hasa katika suala la usafiri wa baharini, kwani ni sekta imeonekana kuwa na changamoto kubwa.



