Mheshimiwa Saidi Yakubu, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mheshimiwa Azali Assoumani, Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro tarehe 2 Julai, 2024. Baada ya tukio hilo muhimu, Mheshimiwa Balozi alipata fursa ya kufanya mazungumzo mafupi na Mheshimiwa Rais Azali Assoumani ambapo aligusia dhamira ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Visiwa vya Comoro kwa kuzingatia masilahi mapana ya nchi mbili hizo. 

Alibainisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kuchangia maendeleo nchini humo. Alijulisha sekta binafsi kutoka Tanzania ipo tayari kushirikiana na Comoro katika kufanikisha miradi mbalimbali katika sekta ya huduma, ujenzi, kutatua changamoto za kibiashara zinazozikabili nchi mbili hizo. 

Naye, Mheshimiwa Rais Azali Assoumani alimpongeza Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu kwa kuteuliwa kumuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan nchini humo kwa kuwa nchi yake in historia kubwa na Tanzania. Alidokezea kuwa Tanzania ilisaidia kupigania uhuru wa nchi hiyo na imekuwa mstari wa mbele kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali.