Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Tanzania uliwasili Visiwani Comoro kwa ajili ya kushiriki mkutano wa wafanyabiashara baina ya nchi hizo mbili (B2B Meeting) uliofanyika kuanzia tarehe 09-11 Julai, 2019. Mkutano huo ambao uliratibiwa na Ubalozi wa Tanzania Visiwani Comoro kwa kushirikiana na kampuni ya CoSo Marketing ulilenga kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na wenzao kutoka Comoro ili waweze kubadilishana taarifa za kibiashara na kuibua fursa mpya za ushirikiano.
Mkutano huo ulishirikisha wafanyabiashara 28 kutoka Tanzania ambao wanawakilisha sekta mbalimbali ikiwemo sekta za mifugo, uzalishaji wa mboga mboga, viwanda vidogo vidogo, uzalishaji mayai n.k. kwa upande wa Comoro zaidi ya wafanyabiashara 60 walishiriki katika mkutano huo.
Huu unakuwa ni mkutano wa tano wa B2B kufanyika baina ya Tanzania na Comoro ambapo mara ya mwisho mkutano wa aina hiyo ulifanyika mwaka 2009. Wakati wakiwa Visiwani hapa wajumbe kutoka Tanzania walipata fursa ya kutembelea maeneo ya biashara na kujionea wenyewe hali halisi ya mazingira ya biashara Comoro, mahitaji ya bidhaa za kila siku pamoja na utambuzi wa bei.
Tarehe 10 Julai, 2019 wajumbe walishiriki katika sherehe za ufunguzi wa mkutano huo zilizofanyika katika Hotel Retaj nje kigodo ya mji wa Moroni. Mgeni rasmi kutika sherehe hizo alikuwa ni Waziri wa Biashara wa Comoro, Mhe. Mohamed M’saidie, aidha wageni wengine waalikwa walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Rais wa Chamber of Commerce ya Comoro, Ndg. Ahmed Bazi, Rais wa Chamber of Commerce wa Anjouan, Ndg. Soyad Mohamed, Rais wa Chamber of Commerce ya Ngazidja, Ndg. Soibroi Eddine Mohamed Balozi wa Sudan, Mhe. Issam Muhi El Dine Khalili na Kaimu Balozi kutoka Ubalozi wa Afrika Kusini Bi. Chwane Nomcebo Valentia Mthethwa.
Aidha, wajumbe walipata fursa pia ya kushiriki kwenye maonyesho ya biashara ya bidhaa kutoka Tanzania ambapo wajasiriamali kutoka Tanzania walipata fursa ya kuonyesha, kuuza na kutangaza bidhaa zao. Sambamba na hilo wajumbe waliweza pia kufanya majadiliano ya (B2B) na kuweza kuingia makubaliano ya kufanya biashara na Wakomoro. Aidha sekta ambazo zimeonekana kuchangamkiwa zaidi ni sekta ya ufugaji wa kuku, mayai, bidhaa za mboga mboga na biashara ya nyama ya Ng’ombe.
Katika hotuba yake Mhe. Balozi aliwahakikishia wafanyabiashara kutoka Tanzania kuwa Ubalozi utaendelea kufanya kazi kwa bidii katika kuratibu shughuli za biashara baina ya Tanzania na Comoro pamoja kuwashauri wafanyabiashara hao kufika Ubalozini pindi watakapo kabiliwa na changamoto za aina yoyote ile.






