Leo tarehe 27 Juni, 2019 Mhe. Sylvester M. Mabumba, Balozi wa Tanzania Visiwani Comoro ameenza ziara rasmi ya kikazi ya siku 4 katika Kisiwa cha Anjouan. Wakati akiwa Kisiwani Anjouan Mhe. Balozi anatarajiwa kukutana na Viongozi mbalimbali wa Kisiwa hicho akiwemo Mhe. Anissi Chassidine, Gavana wa Kisiwa Anjouan, Mratibu wa Shughuli za Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa Biashara.

Sambamba na hilo Mhe. Balozi anatarijiwa kufanya zaira katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji Visiwani hapa ikiwemo kutembelea Maghala ya kuhifadhi Karafuu, Hospitali ya Bambao Mtsanga, Bandari ya Anjouan pamoja na kutembelea mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme unaoratibiwa na kampuni ya Vigor kutoka Tanzania.

Wakati akifanya majadiliano na Mhe. Chamssidine, Gavana wa Kisiwa cha Anjouan Mhe. Balozi alichukua fursa hiyo kumpongeza Kiongozi huyo kwa kuchaguliwa kwake kufuatia kukamilika kwa zoezi la Uchaguzi wa Magavana hapo tarehe 26 Aprili, 2019. Aidha, Mhe. Balozi alimhakikishia Kiongozi huyo utayari wa Tanzania kushirikiana na Anjouan katika masuala ya biashara kwani wafanyabiashara waliowengi hutoka katika Kisiwa hicho.

Sambamba na hilo Mhe. Balozi ameiomba Serikali ya Anjouan iwe inanunua mahitaji yake yote ya chakula hususan mchele kutoka Tanzania badala ya kwenda nchi za Mashariki ya Kati. Aidha, Mhe. Balozi alionyesha utayari wa Tanzania katika kusaidia Anjouan kwenye mafunzo ya Kiswahili na Ufundi Stadi kama sehemu ya kupambana na tatizo la ajira kwa vijana.

Kwa upande wake Mhe. Gavana alichukua fursa hiyo kuelekeza shukrani zake kwa Balozi pamoja na kumkaribisha Anjouan. Kuhusu ushirikiano na Tanzania Mhe. Gavana alionyesha utayari wake na kueleza kuwa siku zote amekua ni muumini wa ujirani mwema na kwamba jirani mzuri wa Comoro kwa sasa ni Tanzania. Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa kuwepo na meli ya uhakika kuratibu biashara hiyo. Aidha, alikaribisha walimu wa Kiswahili na ufundi Stadi kutoka Tanzania na kuelezea kuwa ajenda yake kubwa katika Uongozi wake ni kutafuta ufumbuzi wa suala la ajira kwa vijana.