Dkt. Daniel Mushi, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi - Tanzania ameongoza ujumbe wa watendaji wa Wizara hiyo kutembelea nchini Comoro tarehe 7 - 11 Oktoba 2023 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika biashara ya mifugo, nyama na mazao ya mifugo.
Wakati wa ziara hiyo Dkt. Daniel Mushi alionana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo na Mazingira. Kadhalika, Ujumbe huo ulifanya mazungumzo na Mamlaka ya Kitaifa ya Utafiti wa Kilimo, Uvuvi na Mazingira (INRAPE) ambapo walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika kuratibu biashara ya mifugo, magonjwa ya mifugo, pamoja na ushirikiano kati ya Taasisi. Hivyo, Viongozi hao walikubaliana kukamilisha taratibu za kusainia Makubaliano ya Ushirikiano baina ya Taasisi zao.
Katika hatua nyingine, Ujumbe huo ulikutana na Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara, Wenye viwanda na Wakulima na kubainisha mikakati iliyowekwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha biashara ya mifugo na kulinda afya za mlaji. Ujumbe huo uliwahakikishia wafanyabiashara kwamba watawapatia ushirikiano stahiki kuhakikisha wanaendelea kufanya biashara na Tanzania.
Aidha, Ujumbe ulikutana na Jumuiya ya Wakulima, Wafugaji na Sanaa ikiongozwa na Mwenyekiti wao Bwana. Abdillahi M'Saidie. Wakati wa mazungumzo yao, Viongozi hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano na kutatua changamoto zinazowakabili wanachama wao upande wa Tanzania. Baadhi ya changamoto hizo ni usalama mdogo katika eneo la kusubiria mifugo bandari ya Dar es Salaam na Kwala.