Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Dkt. Daniel Mushi akiambatana na Ujumbe wake pamoja na Watendaji wa Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro wametembelea Bandari ya Moroni tarehe 10 Oktoba 2023. Lengo la matembezi hayo ni kukagua eneo la kushushia mifugo hai inayoingizwa nchini humo kutoka pwani ya Tanzania.
Kadhalika, Ujumbe huo ulitembelea eneo la kuhifadhia kontena za baridi na kujionea miundombinu iliyowekwa katika bandari hiyo kwa ajili ya kupokea na kusafirisha bidhaa zinazoharibika (perishable items) ikiwemo nyama na mazao ya baharini.
Kwa upande wao, watendaji katika Bandari ya Moroni walijulisha kwamba Bandari hiyo haina eneo maalum la kusubirishia mifugo. Hivyo, meli zinazoingia na mifugo hai hupewa kipaumbele cha kushusha mifugo ili iweze kuondoshwa mapema iwezekanavyo na kuondosha usumbufu unaoweza kuepukika. Aidha, walijulisha kuwa kuna changamoto ya meli nyingi kusababisha hasara kwa kuua mifugo kabla ya kuwasili Bandarini, hivyo wameshauri Mamlaka za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kulitafutia ufumbuzi tatizo la meli ya uhakika ya kusafirishia mifugo.
Ziara ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania imefanyika ili kujibu kiu ya wafanyabiashara wa sekta hiyo waliowahi kufikisha changamoto zao Ubalozini wakiomba kupatiwa ufumbuzi. Ubalozi unaendelea kuwasiliana na Jumuiya ya wafanyabiashara na wafugaji kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa.