Prof. Eliamani Sedoyeka, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha amefanya ziara ya kikazi nchini Comoro tarehe 3 - 6 Novemba, 2024 kufuatia mwaliko kutoka kwa Dkt. Ali Ibouroi Tabibou, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Comoro. Wakati wa ziara hiyo, Prof. Eliamani Sedoyeka na Ujumbe wake walipata fursa ya kutembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini humo kwa lengo la kujitambulisha kwa Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu. 

Wakati wa mazungumzo hayo, Prof. Eliamani alijulisha kwamba wametembelea Comoro ili kuangalia fursa ya kuendeleza ushirikiano katika sekta ya elimu hasa kuanzisha masomo katika ngazi mbalimbali kwa njia ya masafa ili kuwapatia fursa raia na wakazi wa Comoro kujiendeleza kimasomo katika maeneo yao ya kazi. Alifahamisha kuwa Chuo cha Uhasibu Arusha kinaendesha mafunzo katika fani zaidi ya 58, hivyo ujio wao nchini Comoro unatarajiwa kuwapatia tija wananchi wote.