Kufuatia mwaliko kutoka Ubalozi wa Tanzania Visiwani Comoro, ujumbe kutoka Shirika la Bima la Zanzibar (Zanzibar Insurance Cooperation- ZIC) ulifanya ziara ya siku tano Visiwani kuanzia tarehe 21 – 25 Februari, 2019. Dhumuni la ziara hiyo ilikuwa kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa Shirika hilo kufungua Tawi lake Visiwani Comoro.

Ziara hii inafuatia ahadi iliyotolewa na Rais wa Zanzibar, Mhe. Dr. Ali Mohamed Shein wakati wa Kongomano la Pili la biashara baina ya Tanzania na Comoro lilofanyika Visiwani Zanzibar Novemba, 2016 ambapo Mhe. Rais Shein alielekeza mashirika ya Serikali ya Zanzibar yaangalie uwezekano wa kufungua operesheni zao Comoro.

Ujumbe huo uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa (ZIC) Bw. Abdul Hashim Amin, aidha wajumbe wengine waliokuwemo katika ziara hiyo ni Bw. Iman Ali Makame. Zonal Manager na Bw. Said Basleym. Wakati wakiwa ziarani wajumbe walipata fursa ya kuona na kufanya mazumgumzo na Balozi wa Tanzania Visiwani Comoro, Mhe. Sylvester M. Mabumba, aidha wajumbe waliweza kuonana pia na mashirika ya Bima yenye operesheni zao Comoro kama Shirika la Al-Amana na Alliance Insurance.

Wajumbe walipata fursa pia ya kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Idara ya Fedha, Ukaguzi na Bima ambaye ndio mratibu wa Sekta ya Bima kwa upande wa Serikali. Kupitia kikao hicho wajumbe walielezwa kwamba Sekta ya Bima Visiwani Comoro bado ni changa na kwamba mpaka sasa ni makampuni 25 tuu ndio yana operesheni zake. Aidha, wajumbe walielezwa kuwa mamlaka hiyo ina miaka miwili tuu tangu ifunguliwe kufuatia mapendekezo kutoka (World Bank na IMF). Hata hivyo, imelezwa kuwa fursa za biashara ya Bima zipo za kutosha na kwamba ZIC imekaribishwa pia katika kutoa mafunzo na kujenga uwezo Serikali ya Comoro katika Sekta hiyo muhimu.