Msanii wa kizazi kipya Mboso aliwasili Visiwani Comoro Tarehe 11 Aprili, 2019 ambapo alitarajiwa kufanya (show) ya aina yake Visiwani hapa tarehe 13 Aprili, 2019. Msanii huyo wa Bongo Fleva aliongozana na ujumbe wake wa watu wanne akiwemo Meneja wake Bi. Sandra.
Wakati akiwa Visiwani hapa msanii huyu na ujumbe wake waliweza pia kukutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania Visiwani Comoro, Mhe. Sylvester M. Mabumba tarehe 12 Aprili, 2019. Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi alichukua fursa hiyo kumpongeza Mboso na timu yake kwa uamuzi wao wa kuja kufanya show Comoro. Aidha, aliwaasa kuwa Mabalozi bora kwa Tanzania na kuiwakilisha nchi vizuri, kwani Tanzania ina mahusiano mazuri na Comoro.
Naye kwa upande wake Mboso alionyesha shukurani zake kwa Ubalozi kwa kumpokea yeye na timu yake na kuonyesha kuwa amefarijika sana na mapokezi hayo. Aidha, aliahidi kuwa atajitahidi kuwa mfano bora kwa Taifa.

