Mheshimiwa Kanali Ahmed Abass Ahmed, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara - Tanzania amefanya ziara ya kikazi katika kisiwa cha Ngazidja nchini Comoro tarehe 13 - 18 Desemba, 2022. Wakati wa ziara hiyo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa aliungana na Mheshimiwa Pereira A. Silima, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Comoro kushiriki ufunguzi wa maonesho ya biashara ya bidhaa na huduma za Tanzania siku ya tarehe 14 Desemba, 2022. Maonesho hayo yalifanyika kuanzia tarehe 12 - 19 Desemba, 2022 katika eneo la Tanzania lililopo mtaa wa Coulee EGT, MORONI.
Kadhalika, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alionana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Sitti Farouata Mhoudine, Gavana wa Kisiwa cha Ngazidja tarehe 16 Desemba, 2022. Wakati wa mazungumzo yao, Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kiuchumi na kijamii baina ya kisiwa cha Ngazidja na Mkoa wa Mtwara. Baadhi ya sekta za kipaumbele zilizojadiliwa ni pamoja na sekta ya elimu ya ufundi, kilimo na kuongezea thamani mazao ya kilimo, uzalishaji, utalii, afya, na ushirikiano baina ya manispaa.


