Mheshimiwa Brig. Jen. Marco E. Gaguti, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara amefanya ziara ya kikazi nchini Comoro kuanzia tarehe 8 hadi 12 Mei 2022. Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alifungua Maonesho ya Biashara na Huduma za Tanzania nchini humo katika hafla iliyofanyika tarehe 10 Mei 2022. Wakati wa hotuba yake, Mheshimiwa Brig. Jen. Marco E. Gaguti alibainisha mikakati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuitumia bandari ya Mtwara kusafirishia mizigo inayoingai Comoro. 

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alifahamisha kuwa Serikali inaendelea kuweka mikakati imara itakayosaidia kufikiwa lengo hilo. Alibainishwa kwamba baadhi ya mikakati hiyo ni kuimarisha mazingira katika bandari, kutoa ghala za kuhifadhia mizigo bila ya malipo, pamoja na kutenga eneo la kupumzishia mifugo kabla ya kusafirishwa. Kadhalika, alifahamisha kuwa Serikali ya Mkoa huo itafuatilia kupatikana meli yenye vyumba vya baridi kumi na mbili (12) ambayo itaweza kutumika kusafirishia nyama na bidhaa mbichi. 

Aidha, wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Sitti Farouatta Mhoudine, Gavana wa Kisiwa cha Ngazidja ambapo walikubaliana kuanzisha ushirikiano wa kikazi baina ya pande mbili hizo katika nyanja za kiuchumi na kijamii.