Kaimu Balozi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro, Bw. Thabit A. Khamis alifanya kikao na ujumbe kutoka Benki ya Ushirika ya Comoro ijulikanayo kwa MECK (Mutuelle d’Epargne et de Credit ya Komor) – Moroni. Ujumbe huu uliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Bi. Laila Said Hassane.

Mkutano huo ulifanyika katika ofisi ya Ubalozi iliyopo mtaa wa Oasis, Moroni ambapo moja ya dhumuni la mkutano huu ilikuwa ni kuangalia maeneo ya ushirikiano wa biashara baina ya Tanzania na Comoro na kuangalia namna gani nchi hizo zinaweza kusaidia wajasirimali wadogo wadogo katika kuratibu baisahra zao hasa wale wanao chukua mikopo ya biashara kutoka Benki hiyo.

Sambamba na hilo Bi. Layla Said Hassane alieleza kuwa Benki yake kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ufaransa na Umoja wa Ulaya wapo katika harakati ya kuzindua mradi wa kukopesha wajasiriamali hasa vijana na kutoa mtaji wa kuendesha mradi wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Mkurugenzi huyo alieleza kuwa Benki yake imetenga zaidi ya KMF 50 Milioni kwa ajili ya kukopesha vijana kuendesha mradi huo pamoja na kutengeneza mtindi. Bi. Laila Said Hassane aliomba Ubalozi kusaidia katika kutafuta shirika kutoka Tanzania ambao wanaweza kuleta ng’ombe wa maziwa pamoja na vifaa vya kutengeneza mtindi.

Kwa upande wake Kaimu Balozi alimpongeza Mkurugenzi huyo kwa hatua ya mradi huo na kumuahidi kuwa Ubalozi wetu utashirikiana na yeye katika kufanikisha mradi huo.