Mheshimiwa Pereira A. Silima, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro amefanya ziara ya kikazi katika Kisiwa cha Anjouan tarehe 26 - 28 Februari 2024. Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Balozi Pereira alionana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Anissi Chamsidine, Gavana wa Kisiwa; alikutana na Uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye viwanda na Wakulima; pamoja na kuonana na wawakilishi wa wafanyabiashara. 

Mheshimiwa Balozi alitumia fursa hiyo kuhakikisha ushirikiano kwa Kisiwa cha Anjouan katika maeneo ya kijamii na kiuchumi ikiwemo biashara, kilimo na uwekezaji. Aidha, alitumija mazungumzo na Viongozi hao kujulisha kuhusu Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Dar es Salaam yatakayofanyika kuanzia tarehe 28 Juni 2024 - 13 Julai 2024 katika jiji la Dar es Salaam. Hivyo, aliwakaribisha wafanyabiashara kutembelea maonesho hayo na kuwaalika wajasiriamali na wazalishaji kushiriki maonesho hayo kuonesha na kutangaza bidhaa zao.