Mhe. Sylevester M. Mabumba, Balozi wa Tanzania Visiwani Comoro alifanya kikao na Umoja wa Watanzania waishio Comoro (TADICO) tarehe 21 Oktoba, 2018. Mkutano huo ulifanyika katika chumba cha mkutano wa Ubalozi; uliopo mtaa Wa Oasis.

Huu ulikuwa ni Mkutano wa pili baina Mhe. Balozi na TADICO tangu kuchaguliwa kwa Viongozi wapya wa Jumuiya hiyo. Mhe. Balozi aliitisha kikao hicho kufuatia machafuko ya siasa yaliyo jitokeza Visiwani hapa kwa upande wa Kisiwa cha Anjaoun.

Katika kikao hicho, Mhe. Balozi aliwaeleza wajumbe kuwa Ubalozi wake unatekeleza wajibu wa kuwahabarisha wanadiaspora juu ya hali ya Ulinzi na Usalama iliopo Visiwani Comoro, ili kila Mtanzania aweze kujihadhari na kuchukua hatua stahiki za kujilinda.

Mhe. Balozi aliwatahadharisha Watanzania kutokujihusisha na masuala yoyote ya siasa yanayoendelea Comoro; pamoja na kukumbushia wale ambao hawajajisajili Ubalozini basi wafanye hivyo mara moja ili Ubalozi uwe unakumbukumbu sahihi za Watanzania waishio Comoro.

Sambamba na hilo, Mhe. Balozi aliwaomba Watanzania hao kuwa katika kipindi hiki wawe wanatembea kwa makundi na vile vile kuhakikisha kwamba wana beba Hati za Kusafiri (Passport) zao; mahala popote wanapo kwenda. Aidha, Mhe. Balozi aliwaomba wale Watanzania ambao hawana shuguli maaluum kwa sasa sio vibaya kwamba katika kipindi hiki wakarejea nyumbani mpaka pale hali ya siasa itakapo kaa sawa.

Mhe. Balozi alikumbushia pia kuhusu umuhimu wa kuwa na mikataba ya kazi hasa kwa Watanzania ambao wanafanya kazi za vibarua katika mashamba ya Wakomoro. Wakati akifunga kikao hicho, Mhe. Balozi alichukua fursa hiyo pia kuwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi na kushiriki kwenye sherehe za kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambapo kwa hapa Comoro sherehe hizo zilipangwa kufanyika tarehe 27 Oktoba, 2018, Palais du Peuple hapa Moroni.