Kikundi cha Afisa mmoja na Askari 14 kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kimetembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro na kukutana na Mheshimiwa Pereira A. Silima, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro tarehe 5 Julai 2022. Kikundi hicho kimewasili nchini humo tarehe 2 Julai 2022 kwa lengo la kuungana na Jeshi la Comoro katika Gwaride rasmi linaloandaliwa kuadhimisha miaka 47 ya Uhuru wa Muungano wa Visiwa vya Comoro tarehe 6 Julai 2022. Katika miaka ya hivi karibuni, jeshi la Comoro limeanzisha utaratibu wa kulialika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kushiriki katika Maadhimisho ya Uhuru wa nchi hiyo. Hii ni mara ya pili kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kushiriki sherehe za namna hiyo.