Mheshimiwa Saidi Yakubu, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Visiwa vya Comoro amekutana na kufanya mazumgumzo na Mheshimiwa Azali Assoumani, Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro tarehe 16 Januari, 2025, Ikulu nchini Comoro. Lengo la mazungumzo hayo ni kubainisha mikakati na mipango ya ushirikiano kati ya Mataifa hayo kwa mwaka 2025.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu alimshukuru Mheshimiwa Rais Azali Assoumani na Serikali yake kwa ushirikiano aliopatiwa mwaka 2024. Alijulisha kuwa ushirikiano huo umeuwezesha Ubalozi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu. Alibainisha  katika kipindi cha kuanzia mwezi Mei hadi Desemba 2024, Ubalozi ulifanikisha matukio mbalimbali zenye tija kwa wananchi kutoka nchi mbili hizi. Mwezi Julai 2024, Tanzania na Comoro ziliratibu Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiao ambapo mikataba mbalimbali ilisaniwa. Kadhalika, Mheshimiwa Balozi alitolea mfano kuwa Ubalozi uliratibu Kongamano la Biashara na Uwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo na usafirishaji ambapo wafanyabiashara na wajasiriamali walipata nafasi ya kubuni mikakati ya kushirikiana.  

Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu alibainisha malengo ya Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro kwa mwaka 2025 katika hatua ya kuimarisha ushirikiano katika Nyanja za kiuchumi na kijamii. Alibainisha kuwa Tanznaia imejipanga kuimarissha ushirikiano katika sekta za kimkakati ikiwemo kuvutia wawekezaji pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binfasi kutoka nchi mbili hizi. Vile vile, alibainisha kuwa Tanzania ipo tayari kuipatia Comoro vitabu na nyenzo za kufundisha somo la Kiswahili iwapo somo hilo litatambuliwa katika mtaala.

Naye Mheshimiwa Rais Azali Assoumani alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Ubalozi katika kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kiuchumi na kijamaii. Alibainisha kuwa juhudi zinazochukuliwa zinathibitisha undugu uliopo kati ya wananchi kutoka Mataifa haya. Alihimiza Ubalozi kuendelea kuvutia wawekezaji kutoka Tanzania kuhamishia shughuli zao nchini Comoro ili kusaidia maendeleo.

Akigusia suala la lugha ya Kiswahili, Mheshimiwa Rais alibainisha kuwa Tanzania ni rafiki wa kweli kwa Comoro. Hivyo Serikali yake itaendelea kuimarisha ushirikiano katika Nyanja mbalimbali ikiwemo kufundisha somo la lugha ya Kiswahili. Alibainsiha kuwa lugha ya Kiswahili itasaidia kuunganisha wafanyabiashara wananchi wa Comoro wanaotembelea Tanzania.

Mazungumzo baina ya Mheshimiwa Rais Azali Assoumani na Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu yamethibitisha azma na nia ya dhati iliyonayo Serikali ya Comoro katika kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Tanzania. Hali hii inabainisha fursa zilizopo kwa raia wa Mataifa haya mawili kuendeleza miradi ya uzalishaji na kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali.