Mhe. Sylvester M. Mabumba, Balozi wa Tanzania Visiwani Comoro, leo alikutunana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uganda na Balozi wa Indonesia wenye makaazi yao nchini Dar Es Salaam, Tanzania.
Balozi Mhe. Richard Tumusime wa Uganda na Balozi Mhe. Dr. Ratlan Pardede wa Indonesia wamekuja Visiwani Comoro kwa ajili ya kuwasilisha hati zao za uwakilishi kwa Mhe. Azali Assoumani, Rais wa Jamhuri wa Comoro.
Katika mazungumzo yao Mhe. Balozi aliwashukuru Mabalozi hao kwa kuja ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha ambapo alichukua fursa hiyo pia kuwa pongeza kwa kukabidhi hati zao za uwakilishi. Aidha, Mhe. Balozi alionyesha utayari wake wa kutaka kushirikiana na Mabalozi wa nchi hizo katika nyanja mbalimbali hasa katika Sekta ya Usafirishaji ambapo alieleza kuwa Tanzania inafanya biashara sana na Visiwa vya Comoro, hivyo wanaweza kubadilishana uzoefu wa kuongeza ufanisi kwenye biashara hiyo.
Kuhusu hali ya siasa Visiwani Comoro, Mhe. Balozi Mabumba aliwahakikishia Mabalozi hao kuwa licha ya changamoto za kisiasa zilizoibuka wiki mbili zilizopitia kwa ujumla hali ya amani na utulivu Visiwani Comoro ipo vizuri na kwamba wananchi wa Visiwani hivyo wanaendelea na shughuli zao za kila siku.
Mhe. Balozi alimalizia kwa kuwa shukuru Mabalozi hao na vile vile kuwaomba waangalie uwezekano wa kufungua ofisi zao za Ubalozi Visiwani hapa.




