Mheshimiwa Pereira A. Silima, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro ameshiriki hafla ya uzinduzi wa kuunganisha huduma za kibenki kati ya matawi ya Benki ya Exim yaliyopo nchini Tanzania na nchini Comoro siku ya tarehe 6 Septemba 2022. Wakati wa tukio hilo, Bw. Aman Hussein, Afisa Uhusiano Benki ya Exim Comoro alitoa maelezo ya kitaalamu na kubanisha kuwa huduma hiyo inawawezesha wateja wa Benki hiyo kupata huduma mbali mbali na kufanya miamala kupitia akaunti zao wakiwa upande wowote katika nchi mbili hizi. Kuanzia sasa ukiwa na akaunti ya Benki ya Exim unaweza kupata huduma katika nchi mbili hizi bila ya usumbufu wowote. Ilifahamishwa kuwa hatua hiyo pia itasaidia kulinda fedha za wateja na wananchi mbali mbali wanapotaka kusafiri kati ya nchi mbili hizi kufanikisha shughuli zozote. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Balozi Pereira A. Silima alipongeza hatua iliyofikiwa na Benki ya Exim kuanzisha huduma hiyo muhimu kwa wateja na wananchi katika nchi mbili hizi. Alifahamisha kuwa kwa kipindi kirefu biashara kati ya nchi mbili hizi ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya usafirishaji bidhaa na kutuma fedha. Hali hiyo iliwafanya wananchi kusafiri na bahasha za fedha na hivyo kuhatarisha usalama wao pamoja na mali zao. Alijulisha kuwa hatua ya kuanzisha huduma hiyo itaimarisha mazingira ya biashara kati ya nchi mbili hizi. 

Vile vile, Mheshimiwa Balozi Pereira alishauri Benki ya Exim kuangalia fursa zaidi zinazopatikana katika utekelezaji wa mikakati ya ushirikiano baina ya Tanzania na Comoro.  Mheshimiwa Balozi alifahamisha kuwa sekta binafsi na kiungo muhimu katika kuleta maendeleo ya nchi. Hivyo, alisisitza kuwa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utaendelea kushirikiana na sekta chini Comoro ili kubuni mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi mbili hizi pamoja na kuanzisha ushirikiano na sekta binafsi katika kufikia malengo ya nchi na wananchi kwa ujumla. 

Hafla ya uzinduzi wa Huduma Shirikishi ya Benki ya Exim ilihudhuriwa na viongozi na watendaji mbali mbali akiwemo Bw. Chamsoudine AHMED, Mwenyekiti wa Shirikisho la Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye viwanda na Wakulima - Comoro; Bw. Ali Amour, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara na Wenye viwanda Zanzibar; Bw. Kizito Galinona, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabaishara, Wenye viwanda na Wakulima (Mkoa wa Mtwara) akiwakilisha Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania; Wafanyabiashara na wananchi mbali mbali