Mheshimiwa Pereira A. Silima, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekutana na wanafunzi walioshiriki shindano la uandishi wa Insha na Usomaji wa Makala lililofanyika tarehe 7 Julai 2022 wakati wa Maadhimisho wa Siku ya Kiswahili Duniani. Tukio hilo lililofanyika katika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro tarehe 7 Septemba 2022 pia lilishirikisha Wakurugenzi wa Taasisi za elimu zinazofundisha somo la lugha ya Kiswahili ikiwemo Kitivo cha Chuo Kikuu cha Teknolojia Comoro; Shule ya Msingi na Sekondari Mwinyi Baraka; Shule ya Msingi AIMECEZER; Kituo cha Maendeleo Bangoi-kuuni; na Kituo cha Lugha "Star English"

Mheshimiwa Balozi Pereira alitumia fursa hiyo kueleza mikakati ya Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro katika kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini humo. Alitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuhamasisha taasisi za elimu kufundisha somo la lugha ya Kiswahili, kushauri Serikali kulitambua somo hilo katika mitaala ya kitaifa, na kuendesha mashindano ya utamaduni na uandishi. '

Aidha, alijulisha kuwa lugha ya Kikomoro inashabihiana sana na lugha ya Kiswahili hivyo ni rahisi kwa wananchi wa Comoro kujifunza lugha hiyo. Alisisitiza kuwa Ubalozi upo tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha lugha ya Kiswahili inaeneo vyema nchini Comoro. 

Jumla la wanafunzi 47 kutoka Chuo Kikuu Comoro na Shule mbali mbali walishiriki shindano la Uandishi wa Insha na Usomaji Makala.