Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Comoro wameratibu mkutano wa washirika wa maendeleo wa Comoro ulioshirikisha Balozi zote na Taasisi za Kimataifa zenye uwakilishi nchini Comoro na wengineo walioshiriki kwa njia ya mtandao kutokea Nairobi.

Akizungumza katika Mkutano huo,Balozi wa Tanzania nchini Comoro Saidi Yakubu ambaye alikuwa Mwenyekiti Mwenza alieleza hatua mbali mbali ambazo Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi inazifanya ikiwemo kuvutia wawekezaji,kushiriki katika utoaji wa huduma za afya na kuratibu wafanyabiashara wa Comoro wanaokwenda Tanzania na pia kuomba ushirikiano zaidi wa pamoja ili kusaidiana na Serikali ya Comoro katika kuharakisha maendeleo yake.

Kwa upande wake,Mwenyekiti Mwenza ambaye pia ni Mratibu Mkati wa Umoja wa Mataifa Comoro,James Tsok Bot aliishukuru Tanzania kwa kukubali uratibu wa mkutano huo unaolenga kujenga uelewa wa pamoja katika wadau wa maendeleo ya Comoro.

Mkutano huo umeshirikisha nchi za Marekani,Libya,Ufaransa,Morocco,Afrika Kusini,taasisi za Benki ya Dunia,Shirika la Afya Duniani,Umoja wa Afrika,Shirika la Maendeleo la Ufaransa,Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Idadi ya Watu,Umoja wa Ulaya na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu ambayo Comoro ni mwanachama wake.