Mheshimiwa Pereira A. Silima, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Comoro amekutana na kufanya mazungumzo na Watendaji Wakuu wa Idara na Vitengo vinavyosimamia uchumi na uzalishaji katika kisiwa cha Anjouani, Wakati wa kikao kazi hicho, watendaji hao walionesha dhamira ya Serikali ya kiisiwa cha Anjouani kuimarisha ushirikiano na mkoa wa Mtwara katika nyanja za elimu pamoja na uzalishaji wa mazao ya kilimo. 

Lengo la kikao hicho ilikuwa ni kupitia maeneo ya ushirikiano yaliyowekwa saini wakati wa ziara ya kikazi ya Mheshiwa Anissi Chamsidine, Gavana wa Kisiwa cha Anjouani iliyofanyika katika mkoa wa Mtwara - Tanzania mapema mwezi Julai, 2022. Watendaji hao walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika kubadilishana uzoefu ili kusaidia kisiwa cha Anjouani kufikia malengo yake katika kuimarisha uzalishaji.